Friday , 29th Jul , 2022

Mbeya City imeendelea kujifua kwa ajili ya msimu ujao, huku Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Anthony Mwamlima akielezea ubora wa nyota wake katika mazoezi yao akiahidi makubwa pale Ligi Kuu itakapoanza, Agosti 17 mwaka huu.

kikosi cha Mbeya City.

Timu hiyo ilianzia mazoezi tangu Jumamosi ya wiki iliyopita, ambapo leo  imeendelea na program licha ya kutokuwa na Kocha Mkuu, baada ya aliyekuwepo Mathias Lule kutimkia Singida Big Stars.

 katika uwanja wao wa mazoezi, Isyesye ilishuhudiwa sura za nyota wapya ambao tayari zimesaini kuitumikia timu hiyo ikiwa ni Tariq Seif, Chesco Mwasimba, Ibrahim Ndunguli na Sixtus Sabilo huku wengine wakitarajiwa kuwasili muda wowote akiwamo Nassor Machezo.

Akizungumza baada ya mazoezi hayo, Mwamlima amesema amefurahishwa na nidhamu ya nyota wake kadri siku zinavyokwenda lakini wanaimarika kiufundi.

Amesema pamoja na kutokuwa na Kocha Mkuu, lakini wanaendelea na program ambapo kesho watasafiri kwa ajili ya mechi yao ya kirafiki dhidi ya Mtibwa Sugar.

"Leo ilikuwa ni mwendelezo wa mazoezi kwa ajili ya msimu ujao, nimeona vijana wanaimarika japokuwa bado hawajakamilika wote ila hivi karibuni tutakuwa tumetimia, usajili bado kama watatu ili kufunga rasmi," amesema Mwamlima.

Hata hivyo imeelezwa kuwa Kocha Mkuu anatarajia kuwasili Jumamosi, ambapo ataungana na timu hiyo mkoani Morogoro kutokea nchini Uganda japokuwa majina yake yameendelea kuwa siri.