Monday , 15th Aug , 2022

Diana Bundala maarufu kama Mfalme Zumaridi ameiomba Mahakama isiendelee kusikiliza kesi yake namba 12 ya mwaka 2022 ya kufanya mkusanyiko usio halali hadi pale atakapopatiwa matibabu

Zumaridi amedai  anasikia maumivu makali mwilini mwake kutokana na kipigo alichopata kutoka kwa Askari Polisi wakati wanamkamata nyumbani kwakwe eneo la Buguku kata ya Buhongwa wilaya ya Nyamagana tarehe 23 mwezi wa pili mwaka huu

Leo upande wa Jamhuri ulileta mashahidi watatu kwa ajili ya kuendelea kutoa ushahidi wa kesi hiyo inayomkabili mfalme Zumaridi na wafuasi wake 84, ndipo kabla mashahidi hao kuletwa Zumaridi akaiambia mahakama hiyo hayupo tayari kuendelea na kesi hiyo kutokana na kusikia maumivu makali mwilini mwake na kwamba viungo vyote pamoja na mifupa vinawaka moto huku bega lake la kushoto likiwa na uvimbe wenye maumivu makali yanayozidi kila siku

Kwa upande wake wakili wa serikali Dorcas Akyoo ameonyesha kushangazwa na Zumaridi kuleta hoja hiyo ya kuumwa leo wakati anadai alipigwa na Askari wakati anakamatwa mwezi wa pili na huu ni mwezi wa nane hivyo akaiomba mahakama kuamua kama wataendelea na shauri au kama watatoa muda wa Zumaridi kwenda kupatiwa matibabu, ndipo hakimu akatoa nafasi kwa mawakili wanaomtetea Zumaridi kuzungumza.

Wakili wa Zumaridi Erick Mutta alipoulizwa na hakimu anayeendesha kesi hiyo Clesensia Mushi kuhusu mteja wake kuumwa akaiambia mahakama kuwa wakileta hoja mahakamani hapo mahakama imekuwa ikiwaelekeza kupeka gerezani bila kutoa maamuzi yoyote huku Wakili Steven kitale nae akisema tarehe 6 ya mwezi huu alipoenda kumuona Zumaridi gerezani alifanikiwa kuzungumza na bibi jela wa gereza kuu la Butimba alipo Zumaridi na anashangaa hadi leo hii Zumaridi hajapelekwa hospitali kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya maumivu yanayomkabili ambayo anadai alipigwa na askari polisi wakati wanamkamata

Hakimu Mushi akataka apate muda wa dakika 30 ili atoe uamuzi wa kuendelea au kutoendelea na kesi hiyo kutokana na hoja ya Zumaridi kudai ana maumivu makali mwilini mwake hivyo kushindwa kuendelea na kesi hiyo hadi  apatiwe matibabu.