Thursday , 1st Sep , 2022

Mkuu wa mkoa wa Kagera Albert Chalamila, ameiagiza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Bukoba (BUWASA), kusitisha huduma kwa taasisi za serikali ambazo zimelimbikiza madeni kwa kushindwa kulipa ankara za maji kwa wakati, na kusababisha mamlaka hiyo kushindwa kujiendesha.

Mkuu wa mkoa wa Kagera Albert Chalamila

Agizo hilo la Mkuu wa mkoa limetokana na taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa BUWASA, wakati wa ziara yake katika ofisi za mamlaka hiyo, kuwa taasisi za serikali zinadaiwa zaidi ya shilingi milioni 100. 

"Waandikiwe barua leo kwamba Mkuu wa mkoa ameagiza wasitishiwe huduma, na sio tu kuagiza bali unukuu hata sheria zako za maji, maana mamlaka inashindwa kujiendesha, mfano haiwezi kununua vifaa, kutandaza mabomba, kufanya ukarabati, kupunguza malalamiko ya wananchi kwa sababu ya madeni makubwa, hizo fedha zinahitajika" amesema Chalamila

Kwa upande wake Mkurugenzi wa mamlaka hiyo John Shilati, amesema kuwa wamepokea maelekezo ya Mkuu wa mkoa na wanakwenda kuyafanyia kazi.