Tuesday , 13th Sep , 2022

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango amewaasa wananchi wa mkoa wa Mwanza na kanda ya ziwa kwa ujumla kuacha kutumia dawa zisizofaa katika katika shughuli za uvuvi ili kuepukana na ongezeko la wagonjwa wa saratani katika ukanda huo.

Dkt. Philip Mpango, Makamu wa Rais Tanzania

Makamu wa Rais amesema hayo leo Septemba 13, 2022 wakati akizindua jengo la wodi ya wagonjwa wa saratani katika hospitali ya rufaa ya kanda ya Bugando iliopo Jijini Mwanza.

Makamu wa Rais ameongeza kwamba takwimu zinaonesha kuwa ugonjwa wa saratani bado ni miongoni mwa magonjwa yanayoongoza duniani kwa kusababisha vifo kwa watu wengi ambapo nchini Tanzania takribani watu 42,000 kila mwaka hupata ugonjwa huo wa saratani huku akisisitiza serikali inawekeza katika ujenzi wa miundombinu ili kuhakikisha huduma za matibabu ya saratani zinasogezwa karibu na wananchi.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema Tanzania imekuwa nchi ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kuanzisha kiwanda cha mionzi dawa kitakachosaidia utoaji huduma kwa wagonjwa wa saratani.