
Athumani S. Amasi, Kaimu Katibu Mtendaji NECTA
Kesho Oktoba 5 na Oktoba 6, 2022 watahiniwa wa mtihani wa kumaliza elimu ya msingi wapatao 1,384,340 wanatarajiwa kuanza kufanya mitihani yao kwa Tanzania Bara katika jumla ya vituo 17,943. Kuelekea zoezi hilo muhimu katika mchakato wa elimu, Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania Bw. Athumani S. Amasi anatoa rai kwa wasimamizi wa mitihani kulinda haki za watahiniwa hasa wenye mahitaji maalum.
“Wasimamizi wahakikishe wanalinda haki ya watahiniwa wenye mahitaji maalum ikiwa ni pamoja na kuwapa mitihani yenye maandishi ya nukta nundu kwa watahiniwa wenye uoni hafifu. Aidha, watahiniwa wote wenye mahitaji maalum waongezewe muda wa dakika 20 kwa kila saa kwa somo la Hisabati na dakika 10 kwa masomo mengine"- Athumani S. Amasi, Kaimu Katibu Mtendaji NECTA.
Aidha, Kuhusu shule binafsi, Baraza la Mitihani la Tanzania linawaonya wamiliki wa shule binafsi kutoingilia majukumu ya wasimamizi, na kwamba Polisi hawatakiwi kuingia kwenye chumba cha mtihani isipokuwa kwa dhararu.
“Baraza linawataka wamiliki wa shule za binafsi wote kutambua kuwa shule zao ni vituo maalum vya mitihani na hivyo hawatakiwi kwa namna yoyote kuongilia majukumu ya wasimamizi wa mitihani katika kipindi chote cha zoezi hilo. Iwapo watabainika kufanya hivyo vituo vyao vitafutiwa, pia baraza linawaasa walimu wakuu, waratibu elimu kata na wamiliki wa shule kutojihusisha katika kupanga na kutekeleza njama za udanganyifu. Kuhusu polisi, wao wanatakiwa kuhakikisha wanasimamia usalama katika eneo linalozunguka kituo cha mtihani, Polisi haruhusiwi kuingia kwenye chumba cha mtihani isipokuwa tu, kama ameitwa na msimamizi kutoa msaada wa dhararu. Narudia, askari haruhusiwi kuingia kwenye chumba cha mtihani"- Athumani S. Amasi, Kaimu Katibu Mtendaji NECTA.