Friday , 7th Oct , 2022

Wananchi wa Kijiji cha Ruvuma Chini, mkoani Ruvuma, wameishukuru serikali kwa kuwapelekea mradi wa maji ambao unagharimu bilioni 1.3 kwani unakwenda kuondoa changamoto ya watumishi wa serikali kukimbia kijijini hapo pamoja na watoto kushindwa kubatizwa kutokana na kukosa majisafi na salama

Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Ruvuma Chini

Wakiongea wakati Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas, alipotembelea kijijini hapo na kukagua mradi wa maji unaosimamiwa na Wakala Wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), ambapo wananchi wa kijiji hicho wamesema wamekuwa na changamoto kubwa ya kukimbiwa na watumishi wa serikali kutokana na changamoto hiyo.

Akiuelezea mradi huo wa maji Mashaka Sinkala, ambaye ni Meneja wa RUWASA wilaya ya Mbinga, amesema ujenzi wa chanzo cha maji tayari umefikia asilimia 90 na imebaki kujenga fensi na kuunganisha bomba.

Baada ya kukagua mradi huo wa maji wa kijiji  hicho, Kanali Laban Thomas, amesema kumekuwa na uharibifu mkubwa wa vyanzo vya maji ambao unaotokana na shughuli za kibanadamu zinazofanywa karibu na vyanzo vya maji, hivyo amewataka viongozi wa serikali kutoa elimu kwa wananchi na kusimamia sheria ya mita 60 kutoka kwenye chanzo cha maji.