Friday , 21st Oct , 2022

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema masuala ya mikutano ya siasa nchini yanahitaji muda wa kutupia jicho sheria mbalimbali zinazosimia suala hilo ili kuepusha madhara yanayoweza kutokea

Amesema sheria na kanuni za mwaka 2019 zinazosimamia mikutano hiyo zinahitaji kutupiwa jicho upya kabla ya kuruhusu kufanyika

Amesema hayo wakati akipokea ripoti ya kikosi kazi alichokiunda cha kuratibu na kuchakata maoni ya wadau wa demokrasia,Jijini Dar es salaam leo Oktoba 21/2022

“Masuala ya mikutano nilisema siku ile ya Demokrasia kwamba masuala ya mikutano yes hakuna anayekataa lakini tukiangalia sheria na kanuni za mwaka 2019 zinataka jicho kwanza, kwahiyo na hizo itabidi tuzitupie jicho kwanza ndio ruhusa itoke” amesema Rais Samia 

Aidha ameweka wazi kuwa kwa sheria zilizopo kwa sasa mikutano ya siasa ikiruhusiwa inaweza kuleta madhara ikiwemo polisi kuingilia na kupiga watu kwa kuwa sheria zinawaruhusu hivyo serikali ina nia njema ya kuzitupia jicho kanuni hizo

“Hatutaki kurudi tulipotoka. Tukifanya mikutano kwa sheria na kanuni hizi Polisi wataingia tena kupiga watu kwa sababu ndivyo sheria inavyomuambia, tunaposema kwamba kanuni lazima tuzitazama sio kwa nia mbaya ni kwa nia njema” 

Katika hatua nyingine Rais Samia amevishauri vyama vya siasa na wadau kutenga muda kwa mwaka mara moja wa kukaa na kujadili masuala yao

“Mijadala ya kisiasa kila mwaka hata mimi ningeomba baraza la vyama vya siasa mfanye hivyo. Kaeni mjijadili na msijadili tu serikali inavyoendesha shughuli za siasa lakini wakati wa kujijadili na nyie wenyewe”

Rais Samia amesema serikali imepokea Ripoti hiyo na inajiandaa kuanza kufanyia kazi mapendekezo mbalimbali yaliyobainishwa