Friday , 21st Oct , 2022

Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Mkoa wa Simiyu, Lupakisyo Kapange, amewaonya watendaji na makampuni ya ukandarasi watakaosimamia ujenzi wa vyumba 60 vipya vya madarasa kwa wanafunzi watakaoingia Kidato cha Kwanza mwakani.

Ni katika kukabiliana na matumizi mabaya ya fedha za umma, ambapo Mkuu wa Wilaya hii ya Bariadi, Lupakisyo Andrea Mjukuu wa Kapange, ameapa kuwashughulikia kwa mujibu wa sheria wale wote watakaojaribu kuhadaa au kutumia isivyo halali, Sh Bilioni Moja zilizotolewa na Mamlaka ya nchi, kwa ajili ya kujenga vyumba vya madarasa kwa wanafunzi watakaoanza masomo yao ya Kidato cha Kwanza, Januari 2023, akisema kamwe moto haulambwi!

“Tumejipanga vizuri kusimamia miradi hiyo kuhakikisha kwamba hakuna mtu atakayechakachua miradi hiyo, mainjinia (wahandiai) tunawataka wasimamie kwa kweli kama utajenga darasa limepasuka mimi nitashughulika na wewe. Lakini hata kule kwenye kata tunataka mamlaka za kata zilizopo kule zisimamie kuhakikisha kwamba hakuna matofali ambayo yana udhaifu, hakuna jingo litakalojengwa dhaifu. Lakini zaidi ya yote sisi wana Bariadi tutashirikiana pamoja kutunza miundombinu ambayo Mhe Rais (Samia) ametuletea katika wilaya yetu” amesema DC Kapange.