
Kuelekea kwenye mchezo huo, Kocha wa timu ya Club Africain, Bertrand Marchand amesema maandalizi yamekamilika huku akiwataja baadhi ya wachezaji nyota wa Yanga ambao anaowahofia kwenye mchezo huo huku akianza na jina la Fiston Mayele.
"Wakati nipo klabu nyingine kabla ya hii miaka miwili nyuma nilihitaji kumsajili kwa sababu alinivutia sana kutokana na aina ya uchezaji wake ila bahati mbaya sikufanikiwa kwa hilo." amesema Marchand.
Kwa upande wa Kocha wa Yanga, Mtunisia Nasreddine Nabi amesema wapo tayari kwa mchezo huo lakini ameweka wazi kuwa, walipeleka barua ya maombi TFF ili mchezo wao dhidi ya Geita Gold usogezwe mbele lakini hawakupata majibu yeyote.
"Mchezo wetu na Geita Gold tuliomba uondolewe ili tupate muda mzuri wa kujiandaa kama ambavyo mashirikisho mengine yanafanya kwa timu zao ila hatuwezi kulalamika sana juu ya hilo kwani akili zetu tunazielekeza kesho kupata matokeo chanya." amesema Nabi.
Klabu ya Yanga inahitaji kupata ushindi wa magoli mengi ili iweke matumaini makubwa ya kufuzu hatua ya Makundi kombe la Shirikisho Barani Afrika kabla ya mchezo wa marudiano dhidi ya Club Africain Novemba 9 mwaka huu katika Uwanja wa Hammedi Agrebi Olympic nchini Tunisia.