Thursday , 3rd Nov , 2022

Serikali imekemea vitendo vya baadhi ya wananchi wanaochunga mifugo na kufanya shughuli za kilimo kwenye maeneo ya hifadhi za misitu ikieleza kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria ya misitu inayokataza kuingiza au kuchunga mifugo kwenye maeneo ya yaliyohifadhiwa.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja

Hayo yamesemwa leo Novemba 3, 2022, Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja(Mb) kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Morogoro Kusini, Innocent Kalogeris aliyetaka kujua ni lini  Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) itaanza kutoa vibali vya malisho kwa wafugaji kama inavyotoa vibali vya kuvuna mbao na mkaa na kuwezesha Serikali kupata mapato.

"Ni dhahiri kuwa kuchunga, kulisha mifugo au kufanya shughuli za kilimo kwenye maeneo ya hifadhi za misitu ni kuvunja sheria, serikali imeyahifadhi maeneo  ya misitu kwa lengo la kulinda rasilimali zilizomo kwa matumizi endelevu ya kizazi cha sasa na kijacho," amejibu Naibu Waziri Mary Masanja