Saturday , 5th Nov , 2022

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Mifugo) Bw. Tixon Nzunda amewataka watendaji serikalini kufanya mabadiliko makubwa ya kifikra, kiutendaji na mifumo ya kiuendeshaji ili kukuza sekta za uzalishaji mali nchini.

Bw. Nzunda amebainisha Mjini Unguja Visiwani Zanzibar, wakati akifungua kikao kilichowakutanisha baadhi ya wataalamu wa Sekta ya Mifugo wa wizara pamoja na taasisi na vitengo vinavyoshughulika na sekta hiyo

“Lazima tuangalie ubora wa mifugo tunayoiandaa, tunayoifuga, mbari za mifugo zenye ubora unaotakiwa, madume yaliyo bora, lakini pia tija kwa maana ya kuongeza uzalishaji likiwemo la uhimilishaji.” Amesema Bw. Nzunda  

Aidha, ameongeza kuwa katika kuhakikisha sekta za uzalishaji mali zinakuwa na tija ni muhimu kuimarisha huduma za mifugo kwa maana ya afya ya mifugo, kinga ya mifugo, udhibiti wa magonjwa na kuimarisha miundombinu muhimu ya huduma ya mifugo.

Pia, katibu mkuu huyo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema kikao hicho cha ushirikiano juu ya Sekta ya Mifugo kati ya watendaji wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni muhimu katika kutatua changamoto zilizopo Visiwani Zanzibar na Tanzania Bara ili kuwa na mwelekeo wa kuimarisha huduma za utafiti na ugani kwa mapana zaidi.