
Aidha tuzo hiyo ni ishara ya kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan katika kuboresha miundombinu ya Afya kwa kujenga wodi nyingi za wazazi, utoaji wa mikopo na vipaumbele vingine kwa ajili ya kuwasaidia wanawake nchini.
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mbeya na Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi, amesema tuzo hiyo iliyotolewa na Umoja wa UWT Mkoa wa Mbeta ni sehemu ya kutambua mchango wa Rais Samia Suluhu katika kuboresha sekta ya maji ambapo kwa sasa huduma ya maji inapatikana kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na ilivyokuwa miaka ya nyuma.
“Zaidi ya Sh. Trilioni 12 zimetolewa na Serikali kwa ajili ya kujenga na kuboresha miradi mbalimbali mkoani Mbeya Mkoa ikiwemo miradi ya maji,ujenzi wa vituo vya afya , ujenzi wa madarasa, pamoja na miundombinu ya barabara, “ amesema Mhandisi Maryprisca na kuongeza
“Mheshimiwa mgeni rasmi ni ukweli ulio wazi kuwa wanawake ndio wanaokwenda zaidi kwenye vituo vya afya kuliko wanaume, mama analijua hili nalo ameweza kutujengea hospitali kubwa za wilaya zote za mbeya kila mmoja imepatiwa bil 500 kwa ajili ya wodi tatu zinazojengwa”Alisema Mahundi
Akizungumza katika kongamano hilo mgeni rasmi Spika wa bunge Dk,Tulia Ackson amewataka viongozi wa UWT kuanzia ngazi ya chini kuwa na utaratibu wa kuandaa mikutano na wananchi ili kuwafahamisha mafanikio miradi inayotekelezwa sambamba na kuchukua kero zao na kuzipeleka kwa viongozi wa ngazi za juu ili kuzifanyia kazi na kuwaletea maendeleo wananchi hao.
Akipokea tuzo hiyo kwa niaba ya Rais Samia Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Homera amewapongeza wanawake wa Mkoa huo kwa kuandaa kongamano hilo la kutambua jitihada zinazofanywa na Serikali, huku akimshukuru Rais Samia kwa ujenzi wa jengo la mama na mtoto kwa ajili ya kujifungulia lililojengwa mkoani humo na kugharimu zaidi bilioni 11.