Friday , 6th Jan , 2023

Baadhi ya madiwani wa manispaa ya Bukoba mkoani Kagera wameiasa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa - TAKUKURU - mkoani humo kuweka mazingira ambayo yatawawezesha kuwa rafiki wa wananchi, badala ya kuwafanya wananchi kuogopa kufika katika ofisi zao kutoa kero zinazowakabili

Wakizungumza wakati wa kikao cha kutoa elimu ya namna ya kupambana na rushwa na kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia programu ya Takukuru Rafiki iliyoanzishwa chini ya ofisi ya Rais, madiwani hao wamesema kuwa wapo wananchi wenye kero lakini wanaogopa kuzitoa kutokana na kutokuwepo ukaribu na wengine kuhofia kuzungushwa.

"Mtu asiogope kuingia kwenye ofisi zenu kutoa kero yake, na akitoa kero ishughulikiwe isiwe kila siku anadhuria utafiri yupo mahakamani, ifanyiwe kazi haraka apate fursa ya kwenda kuendelea na shughuli zake nyingine, hii nenda rudi mara tukikuhitaji tutakuita inagongeza kero, fanyeni kazi kwa weledi" wamesema

Akizungumza katika kikao hicho mkuu wa Takukuru Mkoa wa Kagera, John Joseph amesema kuwa lengo la programu hiyo ni kushirikisha jamii katika kuibua kero za maendeleo na kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayowakabili kwa kushirikiana na taasisi hiyo, wananchi na viongozi.

"Katika elimu tutakayoitoa, tutawajengea uwezo wa kufahamu jinsi gani wanaweza kutambua kero zinazowazunguka kwenye maeneo yao na jinsi gani ya kudhibiti kero hizo, na baada ya kuwapa elimu hiyo tutawaomba wananchi watusaidie kila mdau atakayekuwepo kutaja kero moja tu iliyoko katika eneo lake, kwa siri na sisi tutakwenda kuzichambua" amesema Joseph.