Thursday , 12th Jan , 2023

Jeshi la Polisi mkoani Mwanza, limedhamiria kuwapa mafunzo ya utayari walinzi wa makampuni binafsi ili kuhakikisha wanatekeleza kwa weledi shughuli zao za ulinzi na kuhakikisha wanajua namna ya kutumia silaha wanazopewa kwa ajili ya shughuli zao.

Wilbroad Mutafungwa, Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza

Hayo yamebainishwa katika kikao maalum cha kuweka mikakati ya namna ya kukabiliana na uhalifu kilichowakutanisha wamiliki wa makampuni ya ulinzi na wamiliki wa vituo vya mafuta jijini Mwanza ambapo Kamanda wa Polisi mkoani humo Wilbroad Mutafungwa, akawataka kuhakikisha wanawatengea muda walinzi wao ili waweze kupewa mafunzo maalum ya utayari yatakayowasaidia kupambana kikamilifu na wahalifu

"Unakuta mlinzi wa kampuni analinda sehemu, akitokea mtu anafanya uhalifu basi mlinzi ndiyo anakuwa wa kwanza kukimbia, nawaagiza wamiliki wa makampuni ya ulinzi kuhakikisha wanawatoa walinzi wao ili wapate mafunzo ya utayari kutoka jeshi la polisi ili na wao waweze kufanya shughuli zao vizuri na kuacha kujihusisha na uhalifu," amesema Kamanda Mutafungwa

Katika hatua nyingine Kamanda Mutafungwa akawataka wamiliki wa vituo vya mafuta kuhakikisha wanafunga kamera kwenye vituo vyao ili pindi uhalifu unapojitokeza zisaidie kwenye upelelezi wa kuwabaini wahusika