Sunday , 15th Jan , 2023

Wanaume wanaopendelea kutumia vinywaji vyenye sukari kila siku wapo hatarini kupoteza nywele zao na kuwa wenye viapara.

Kipara

Utafiti huo umefanywa na Chuo Kikuu cha Tsinghua cha nchini China, ambao umeeleza kuwa wanaume wanaopoteza nywele na kuwa vipara kwa siku za hivi karibuni wanahusishwa na unywaji wa vinywaji vingi vyenye sukari.

Utafiti huo uliangalia data kutoka kwa wanaume zaidi ya 1,000 wa China, wenye umri wa miaka 18 hadi 45, kuanzia Januari hadi Aprili 2022 ili kulinganisha tabia za maisha zinazoripotiwa na upotezaji wa nywele.

Waligundua kuwa upotezaji wa nywele ulikuwa karibu ya 30% zaidi ya wanaume ambao walikuwa na tabia ya kila siku ya kunywa kinywaji chenye sukari kama vile vinywaji baridi, juisi, vinywaji vya kuongeza nguvu, vinywaji vya michezo, kahawa na chai iliyotiwa ambapo ni sawa na lita moja hadi tatu kwa wiki.

Wanaume ambao waliripoti kuwa na zaidi ya kinywaji kimoja cha sukari kwa siku walikuwa na uwezekano mkubwa wa kupoteza nywele kwa 42% zaidi ikilinganishwa na wale ambao hawakuwahi kunywa vinywaji vya sukari.

Watafiti pia waligundua kuwa wengi wa washiriki wa utafiti walikunywa angalau baadhi ya vinywaji vyenye sukari katika lishe yao ya kila siku na karibu nusu waliripoti kuwa na vinywaji vyenye sukari zaidi ya mara moja kwa siku.

Utafiti huo umeainisha kwamba tabia za wanaume kunywa vinywaji vyenye sukari sio sababu pekee za upotezaji wa nywele, bali kuna sababu zingine kama vile lishe duni, masuala ya afya, mkazo na matatizo ya afya ya akili.