Wednesday , 8th Feb , 2023

Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limepokea kwa masikitiko kauli iliyotolewa na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa kuwa Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari (MSA 2016), umeshindikana kuingizwa bungeni kutokana na ripoti nyingi za kamati za kisekta za Bunge.

Bungeni

Taarifa hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Jukwaa hilo Deodatus Balile na kusema sababu iliyotolewa ni nyepesi na inapata wasiwasi iwapo kuna utashi wa kufanya mabadiliko katika sheria hiyo kwa kusema katika vikao vilivyotangulia ulikuwepo ugumu kutoka kwa baadhi ya wastaafu walioazimwa na TCRA, maafisa kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, na baadhi ya vyombo vya ulinzi na usalama wakionesha wazi kutokuwa na nia ya kurekebisha sheria hii.

"Tumekuwa na mawasiliano mazuri na Waziri Nape, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mwandishi Mkuu wa Sheria wa Serikali, Onorius Njole na Ofisi ya Bunge, ila maafisa wachache wa chini ndiyo kwa muda mrefu wamekwamisha mabadiliko ya sheria hii, mwanzo tuliahidiwa muswada wa mabadiliko ungeingizwa bungeni mwaka 2022 katika vikao vya Februari, wakasema Aprili, baadaye Septemba, ikasogezwa Novemba, lakini kote huko hakuna kilichotekelezwa," amesema Mwenyekiti wa TEF Deodatus Balile

Aidha Balile ameongeza kuwa, "Muswada huu ungeingizwa bungeni kwa namna ya ajabu, muswada huu umeshindikana kuingia bungeni tena (Februari, 2023), tunajiuliza kama taarifa za kamati zimezuia muswada kuingia bungeni, je, muswada huu utapataje nafasi kwenye mkutano ujao wa Aprili, 2023? je, itawezekana vipi katikati ya hotuba za Bunge la Bajeti la mwaka 2023/2024,".