Friday , 19th May , 2023

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa ametoa wito kwa mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali duniani kushirikiana na makampuni ya mawakala ya utalii katika nchi husika kuwaleta watalii nchini ili kuifikia azma ya kuwaleta watalii milioni tano ifikapo 2025

Mchengerwa ametoa kauli hiyo wakati akisoma hotuba yake kwenye mkutano maalum wa kibiashara baina ya makampuni makubwa duniani ya watalii kutoka nchini China na wadau wa utalii nchini jijini Arusha alipokuwa ameambatana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Anderson Mutatembwa.

Amempongeza Balozi wa Tanzania nchini China kwa kushirikiana na wadau wengine kuratibu ujio wa mawakala hao na kutoa  wito kwa mabalozi wengine  kuiga mfano  huo. 

Amefafanua kuwanchi ya China ni soko la kimkakati la utalii kwa Tanzania kwa kuwa ni miongoni mwa nchi yenye watalii wengi ambao Tanzania inapaswa kunufaika nalo.

Akitolea mfano amesema  kuwa nchi ya China inatoa  takribani watalii milioni 155 kwa mwaka  kwenda  sehemu mbalimbali duniani lakini ni watalii 33000 kutoka china ndiyo wanaotembelea Tanzania kwa mwaka.

Amesema Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Bodi ya Utalii Tanzania na Ubalozi wa Tanzania nchini China wameandaa program maalum hii inayolenga kuwavutia watalii wengi kutoka China kuja kutembelea Tanzania.

Amefafanua kuwa pamoja na mambo mengine program hiyo itahusisha masuala ya mafunzo ya utamaduni, masuala ya lugha, mifumo mbalimbali ya kurahisisha malipo wakiwa nchini, vyakula vya kichina na namna ya kujitangaza.

Aidha, amesema program hiyo itawasaidia watalii  kutoka China kufurahia  utalii wa Tanzania, pia kuratibu safari za kitalii ikiwa ni mwendelezo wa program ya Royal Tour  iliyoasisiwa na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan. Waziri Mchengerwa amesema mawakala hao ikiwa ni kundi lenye ushawishi mkubwa kwenye mnyororo  wa thamani wa utalii  duniani litasaidia pia kufungua milango ya uwekezaji mkubwa kwenye  sekta ya utalii hapa nchini.

 Amewapongeza wadau mbalimbali wa utalii nchini ambao wameshirikiana na Serikali katika  kuratibu ujio huu wa  mawakala hao huku akisisitiza kuwa kwa sasa Serikali itaongoza  katika  kufanya kushawishi  badala  ya kubaki  nyuma kama na kuacha kazi hiyo kufanywa na wadau pekee.

Amesema Tanzania ni nchi iliyobarikiwa kuwa na vivutio vingi vya utalii ambavyo havipatikani katika sehemu nyingi duniani hivyo ina kila sababu ya kuweka mikakati mizuri ili  kuwavutia watalii na wawekezaji ili waje nchini na kuleta fedha za kigeni.

“Ninaamini taifa letu ni taifa la kipekee, taifa ambalo lina vivutio vingi ambavyo mataifa mengi hayana na yanatamani kuwa katika nafasi kama yetu, pia vivutio vyetu ni vivutio ambavyo sehemu nyingi ya dunia havipo na ndiyo maana katika takwimu za UNESCO tunaongoza katika nafasi za juu kabisa. “amesisitiza Mhe. Mchengerwa.

Amewahakikishia mawakala hao kuwa tayari Serikali imeshaainisha maeneo ya uwekezaji katika hifadhi na kwamba  imeandaa mazingira rafiki yatakayowezesha kufanya  biashara na kupata  faida. 

Mara baada ya  mkutano  huu mawakala  hao ambao wameambatana na  vyombo vikubwa habari 6 kutoka nchini  China wataembelea maeneo  ya Hifadhi  ili kuona  vivutio vya utalii  kabla ya kurejea nchini China mwishoni mwa mwezi Mei 2023.