Friday , 23rd May , 2025

Mawaziri wa Fedha na magavana wa Benki Kuu wa Kundi la G7 kwa pamoja wameahidi kushughulikia suala la ukosefu wa usawa katika uchumi wa dunia.

Mawaziri hao wa G7 pia wamekubaliana juu ya uwezekano wa kuongeza vikwazo dhidi ya Urusi.

Waziri wa Fedha wa Canada Francois-Philippe Champagne aliwaambia waandishi wa habari kwamba waliafikiana kwa pamoja juu ya maswala muhimu zaidi ya kiulimwengu yanayowakabili.

Kabla ya mkutano huo kulikuwa na shaka ikiwa kungetolewa taarifa ya pamoja kwa kuzingatia migawanyiko kuelekea ushuru wa Marekani na vita vya Urusi nchini Ukraine.

Mkutano huu unafungua milango ya mkutano wa kilele wa wakuu wa G7, Juni 15-17 katika eneo la mapumziko la mlima la Kananaskis, nchini Canada, ambapo Rais Donald Trump atahudhuria. #EastAfricaTV