
Maandamano makali ya kupinga kupanda kwa bei ya mafuta, yaliyoambatana na uporaji mkubwa wa maduka ya vyakula yamesababisha vifo vya watu 22 nchini Angola.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Manuel Homem ametangaza idadi hiyo mbele ya waandishi wa habari jana Jumatano Julai 30,2025 na kuripoti majeruhi 197.
Uamuzi wa serikali mwanzoni mwa mwezi Julai wa kuongeza bei ya mafuta yenye ruzuku kubwa kutoka kwa kwanza 300 hadi 400 kwa lita (sawa na euro 0.28 hadi 0.38) ulizua hasira kwa watu wengi katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika, nchi ya pili kwa uzalishaji wa mafuta barani Afrika baada ya Nigeria, lakini ambapo watu wengi wanaishi katika umaskini.
Mashirika ya kiraia awali yaliitisha maandamano kila Jumamosi kwa muda wa wiki tatu zilizopita. Kisha, chama cha madereva wa teksi nchini humo kilitangaza mgomo wa siku tatu ulioanza siku ya Jumatatu. Hali ilizidi kuwa mbaya siku ya Jumatatu na Jumanne huku kukishuhudiwa visa vingi vya uporaji.