
Wazalishaji wa maudhui mtandaoni wametakiwa kuchapisha taarifa sahihi za uchaguzi ambazo hazina chembe ya upotoshaji ili kuepuka kuvuruga na kulinda amani na utulivu wa nchi.
Akizungumza leo Agosti 3, 2025, jijini Dar es Salaam, wakati akifungua Mkutano wa Kitaifa kati ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na wazalishaji wa maudhui mtandaoni kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji wa Mahakama ya Rufani Jacobs Mwambegele, amesema kuwa Tume ina matumaini makubwa na vyombo vya habari katika kufanikisha uchaguzi wa mwaka huu kwa kupitia ushiriki wao wa karibu.
Jaji Mwambegele amesema kuwa ana imani kubwa na vyombo vya habari kutokana na ushirikiano walionesha tangu awali kwenye zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, huku akisisitiza kuwa waendelea kuwa wepesi wa kuwasilisha hoja na ushauri kila tunapokutana katika vikao mbalimbali.
Nae Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhan Kailima, akiwasilisha mada kuhusu maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 na nafasi ya vyombo vya habari, amesewasihi, kutumia nafasi na fursa walizonazo kuhakikisha kuna kuwepo na taarifa za mara kwa mara kuelezea yanayoendelea kuhusu uchaguzi mkuu.
Amefafanua kuwa tume imeweka utaratibu wa kushirikisha vyombo vya habari katika hatua zote za uendeshaji wa uchaguzi huu, ili kuweka uwazi na kuhakikisha ushiriki wao wa moja kwa moja.