Monday , 18th Aug , 2025

Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza limemfikisha Mahakamani Kulwa Steven Ibasa (maarufu kama Baba Claud), mwenye umri wa miaka 37 na mkazi wa Nyakato kwa tuhuma za kumlawiti mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka minne.

Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza limemfikisha Mahakamani Kulwa Steven Ibasa (maarufu kama Baba Claud), mwenye umri wa miaka 37 na mkazi wa Nyakato   kwa tuhuma za kumlawiti mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka minne.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka iliyosomwa na Wakili wa Serikali Mwanahawa Changali mbele Hakimu Mkazi Mwandamizi Mhe, Juma Opudo, mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo tarehe 20 na 21 Julai 2025, akiwa nyumbani kwake, maeneo ya Nyakato, ambapo alimuita mtoto huyo sebuleni kwake na kutekeleza kitendo hicho cha kikatili.

Wakili Changali alieleza kuwa mshtakiwa alitumia fursa ya kutokuwepo kwa bibi wa mtoto huyo  ambaye mara kwa mara huhudhuria ibada kanisani hivyo alitumia nafasi hiyo na kumuita mtoto ndani kwake, kisha kumfanyia ukatili huo.

Kesi hiyo nambari 20028/2025 inahusisha shtaka moja la kulawiti, kinyume na kifungu cha 154 (1) (a) (2) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, marejeo ya mwaka 2023.

Mshtakiwa amekana shtaka lililosomwa dhidi yake, ingawa amekiri kumfahamu mtoto husika. Hata hivyo, upande wa mashtaka umeieleza mahakama kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika na kuomba mshtakiwa asomewe hoja za awali.

Katika hoja hizo, ilibainika kuwa mshtakiwa ni jirani wa Bi. Asteria ambaye ni bibi wa mtoto huyo, ambapo alikamatwa mnamo tarehe 21 Julai 2025 na kufikishwa kituo cha polisi Nyakato na Kirumba, kisha kuhojiwa kabla ya kufikishwa mahakamani.

Baada ya kusomewa hoja hizo, Mhe Hakimu amesema kuwa kesi hiyo kwa kuwa ina dhamana,  mshtakiwa alitakiwa kuwa na wadhamini wawili wenye kitambulisho cha taifa, barua ya utambulisho kutoka kwa muajiri, na kila mmoja kusaini hati ya dhamana ya shilingi milioni tano. Hata hivyo mshtakiwa ameshindwa kutimiza masharti hayo, na kupepelekwa rumande hadi Septemba 1, 2025 ambapo kesi hiyo itatajwa tena kwa ajili ya kuanza kusikilizwa kwa upande wa mashahidi.