
Ziara hiyo inanuwia kupunguza mvutano baada ya Israel kuushambulia mkutano wa viongozi wa kundi la Hamas uliokuwa ukifanyika kwenye mji mkuu wa taifa hilo la Ghuba Jumanne iliyopita.
Ofisi ya Rubio imesema mwanadiplomasia huyo atakutana na viongozi wa Qatar na "kuwahakikishia uungaji mkono wa Marekani na kutoa ahadi kwamba shambulizi kama hilo halitotokea tena."
Viongozi mjini Doha wameghadhibishwa na shambulizi hilo na tangu lilipotokea wamekuwa wakitoa mwito kwa jumuiya ya kimataifa kuiwajibisha Israel kwa kile wamekitaja kuwa "kitendo cha kichokozi".
Qatar ambayo kama ilivyo Israel ni mshirika wa karibu wa Marekani, imekuwa mstari wa mbele katika kutafuta suluhu ya vita vya Gaza hasa kupitia ukaribu wake na kundi la Hamas ambalo lina ofisi makao yake mjini Doha.