Tuesday , 21st Oct , 2025

Kuhusu ujenzi wa soko jipya la kisasa katika eneo la Kawe, Dar es Salaam, Dkt. Samia ameahidi kuwajengea soko jipya litakalokuwa la kisasa litakalowawezesha kufanya biashara kwa ubora, usafi na usalama unaotakiwa.

Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuendelea kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo upanuzi wa miradi ya barabara, kuendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maji itakayohakikisha wakazi wa Dar es Salaam, Pwani na Morogoro wanapata huduma ya uhakika ya maji safi na salama, ujenzi wa madaraja ya juu (flyovers) na ujenzi wa soko jipya la Kawe baada ya lile la awali kuungua.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye Viwanja vya Leaders Club, Kinondoni jijini Dar es Salaam, Jumanne, Oktoba 21, 2025, Dkt. Samia amesema katika miaka mitano ijayo serikali yake itakamilisha ujenzi wa Bwawa la Kidunda lenye thamani ya shilingi bilioni 336, mradi ambao unatarajiwa kuhudumia mikoa mitatu ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro.

Ameongeza kuwa sambamba na mradi huo, serikali inakwenda kuanza utekelezaji wa mradi mkubwa wa kutoa maji kutoka Mto Rufiji, ambao unalenga kumaliza kabisa tatizo la upatikanaji wa maji hasa katika kipindi cha kiangazi jijini Dar es Salaam.

Kuhusu ujenzi wa soko jipya la kisasa katika eneo la Kawe, Dar es Salaam, Dkt. Samia ameahidi kuwajengea soko jipya litakalokuwa la kisasa litakalowawezesha kufanya biashara kwa ubora, usafi na usalama unaotakiwa. Pia, ametumia nafasi hiyo kuwapa pole wale waliothirika na kadhia ya kuungua kwa soko hilo.

Dkt. Samia ametumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi kutoka tarehe 29 na kwenda kupiga kura, “Niwahakikishie tarehe 29, kesho kutwa tu mwezi huu wa 10, niwaombe tokeni muende mkapige kura. Ninayeongea hapa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa nchi hii, ninataka niwaambie, maandamano yatakayokuwepo ni ya watu kwenda vituoni kupiga kura, hakuna maandamano mengine yatakayokuwepo hapa, hakuna tishio la kiusalama litakalokuwepo, anayesema ni Amiri Jeshi Mkuu wa Nchi hii.” Amesema.