Kulingana na data kutoka nchi 117 takriban wanawake na wasichana 50,000 waliuawa na wapenzi wa karibu au wanafamilia mnamo 2024
Hii ni kwa Mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Madawa ya Kulevya na Uhalifu na Wanawakem, Ikiwa ni ripoti iliyotolewa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake.
Ripoti hiyo iliongeza kuwa asilimia 60 ya wanawake waliuawa duniani kote na wenzi au jamaa kama vile baba, wajomba, mama na ndugu.
Ripoti ya Umoja wa Mataifa inasema chakusikitisha zaidi ni kwamba hakuna dalili ya hali hii kubadilika na nyumbani kunaendelea kuwa mahali hatari kwa wanawake na wasichana katika suala la hatari ya kuuawa.
Idadi hiyo ni ndogo kuliko takwimu iliyoripotiwa mnamo 2023, ingawa haionyeshi kupungua katika uhalisia, kulingana na ripoti, kwani inatokana na tofauti za upatikanaji wa data kutoka nchi hadi nchi.
Hakuna eneo duniani lililokosa visa vya mauaji ya wanawake, lakini Afrika ilikuwa na idadi kubwa zaidi mwaka jana ikiwa na karibu 22,000, ripoti hiyo ilisema.
Ripoti hiyo ilisema maendeleo ya kiteknolojia yamezidisha aina fulani za unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana na kuunda zingine, kama vile kushirikisha picha bila ridhaa, utafutaji taarifa mitandaoni na video za uwongo.




