Thursday , 4th Dec , 2025

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amesema Tanzania imedhamiria kuhakikisha inalinda afya, maisha ya watu na mazingira kwa kutoa kipaumbele katika uimarishaji wa mfumo wa afya.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amesema Tanzania imedhamiria kuhakikisha inalinda afya, maisha ya watu na mazingira kwa kutoa kipaumbele katika uimarishaji wa mfumo wa afya, kuwekeza katika utafiti wa kisayansi, na kuhimiza matumizi ya dawa.

Dkt. Nchimbi ametoa kauli hiyo wakati akifungua Maadhimisho ya Kanda ya Afrika ya Wiki ya Kimataifa ya Usugu wa Vimelea vya Magonjwa dhidi ya Dawa, yanayofanyika Hyatt Regency, Jijini Dar es Salaam.

Amesema hatua hizo ni katika kukabiliana na tishio linaloongezeka la usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa, ambapo pia ametoa wito kwa nchi za Afrika kujiunga katika mapambano hayo ya kimataifa kwa kuunga mkono juhudi za matumizi sahihi ya dawa hizo za kuokoa maisha, kwa kubadilishana ujuzi, kuimarisha ushirikiano na kuhakikisha kwamba dawa za vimelea vya magonjwa zinabaki kuwa na nguvu kwa vizazi vijavyo.

Makamu wa Rais amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa kupitia kubadilishana takwimu na uratibu wa utekelezaji wa sera katika mapambano dhidi usugu wa vimelea vya magonjwa. Amesema ushirikiano huo ni muhimu kwa kuwa maambukizo hayazuiliwi na mipaka ya kijiografia.

Dkt. Nchimbi ameutaja uwekezaji katika uvumbuzi na utafiti kuwa ni muhimu kwa lengo la kuboresha zana mpya za uchunguzi, chanjo na matibabu mbadala ambayo yanaweza kupunguza utegemezi kwa dawa za asili za vimelea vya magonjwa na kuweza kudhibiti mabadiliko ya magonjwa yanayojitokeza kwa jamii moja moja.