Thursday , 4th Dec , 2025

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imeahirisha kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili mwanaharakati wa mitandaoni Mange Kimambi hadi Januari 28, 2026, baada ya upande wa Jamhuri kueleza kuwa upelelezi haujakamilika.

 

Shauri hilo namba 000021172/2025, liliitwa leo Desemba 4, 2025, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Hassan Makube, ambapo upande wa mashtaka uliomba muda zaidi. Hakimu Makube alielekeza upelelezi ukamilike kabla ya tarehe hiyo kwa kesi kuanza kusikilizwa rasmi.

Mange anakabiliwa na shtaka la utakatishaji wa Shilingi milioni 138.5 alizodaiwa kuzipata Machi 2022 kwa kufanya kazi ya uandishi wa habari bila kibali na kutumia vitisho. Kesi hiyo imefunguliwa chini ya Sheria ya Utakatishaji Fedha na Uhujumu Uchumi.

Kwa sasa Mange yupo nje ya nchi, na Serikali imethibitisha kuwa inachunguza uwezekano wa kumrejesha kupitia sheria ya Extradition, huku Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ikitumia mikataba ya kimataifa kufanikisha hilo.