Thursday , 11th Dec , 2025

"Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama vina wahakikishia kuwa vitaendelea kulinda amani na usalama wa nchi pamoja na maisha na mali zenu na tuendelee kutoa wito wa kuzingatia kanuni za kiusalama zinazotakiwa zianze na kila mmoja wetu kwanza"

Jeshi la Polisi nchini Tanzania limewataka Wananchi kuendelea kuwakataa na kuyakataa yale yote yenye mwelekeo wa kichonganishi, uzushi, uongo, yenye kujenga chuki pamoja na yenye kuhamasisha kufanya vurugu na matukio yote yenye viashiria vya kuvunja sheria za nchi.

Taarifa kwa Vyombo vya habari iliyotolewa mapema leo Alhamisi Disemba 11, 2025 na Msemaji wa Jeshi la Polisi, Naibu Kamishna wa Polisi David Misime imesisitiza pia kutosambaza ujumbe wenye kuleta chuki na uchochezi kwa jamii na badala yake kufuta ujumbe wa namna hiyo kwenye Mitandao ya kijamii ikiwemo WhatsApp.

"Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama vina wahakikishia kuwa vitaendelea kulinda amani na usalama wa nchi pamoja na maisha na mali zenu na tuendelee kutoa wito wa kuzingatia kanuni za kiusalama zinazotakiwa zianze na kila mmoja wetu kwanza sambamba na sisi sote kutii sheria." Imesema taarifa hiyo.

Katika hatua nyingine Polisi imeeleza kuwa kila mmoja aendelee kufanya shughuli zake halali bila hofu kutokana na usalama kuendelea kuimarika kote nchini Tanzania kutokana na ushirikiano mkubwa unaoendelea kutolewa kwa Vyombo vya ulinzi na usalama katika kulinda na kuimarisha amani, utulivu na usalama nchini Tanzania.