Friday , 12th Dec , 2025

Ratiba iliyotolewa na Bunge la Tanzania imedokeza kuwa maombolezo yameanza leo nyumbani kwake eneo la Itega Jijini Dodoma

Maombolezo ya aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Peramiho, Marehemu Jenista Joakim Mhagama, yameanza leo Desemba 12 na yatahitimishwa Desemba 16, 2025 wakati mwili wake ukipelekwa katika Kijiji cha Ruanda wilayani Mbinga kwa ajili ya mazishi.

Ratiba iliyotolewa na Bunge la Tanzania imedokeza kuwa maombolezo yameanza leo nyumbani kwake eneo la Itega Jijini Dodoma kabla ya kesho Desemba 13, ibada kuu ya kumuaga marehemu kufanyika katika Kanisa Katoliki Kiwanja cha Ndege Jijini Dodoma, ikihudhuriwa na waombolezaji kutoka maeneo mbalimbali.

Baada ya ibada hiyo, mwili utasafirishwa kuelekea Songea ambapo Desemba 14, maombolezo yataendelea nyumbani kwa marehemu katika eneo la Makambi, Songea Mjini huku jioni ya siku hiyo, mwili ikitarajiwa kupelekwa katika Kanisa Katoliki Matogoro kwa ibada nyingine kabla ya kurejeshwa nyumbani.

Desemba 15, shughuli za kuaga zitaendelea Peramiho, Songea Vijijini, kupitia ibada itakayofanyika katika Kanisa Katoliki la Peramiho, kisha waombolezaji wa eneo hilo watapata nafasi ya kutoa heshima zao za mwisho kabla ya Desemba 16, mwili wake kupelekwa katika Kijiji cha Ruanda wilayani Mbinga kwa ajili ya mazishi.