Tuesday , 30th Dec , 2025

Uamuzi huo umefuatia malalamiko ya abiria waliokuwa wanasafiri na basi hilo kukwama tangu jana Disemba 29 majira ya saa kumi jioni katika eneo la njia Panda ya Himo wilaya Moshi mkoani Kilimanjaro baada ya gari hilo kuharibika.

Dereva wa basi la kampuni ya Makupa lenye namba za usalili T 958 DRK linalofanya safari zake kutoka jiji la Arusha kuelekea Dar es salaam Ibrahim Athumani amekamatwa na Polisi na kuwekwa mahabusu mpaka pale mmiliki wa basi hilo atakapopatikana.

Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Kilimanjaro, ACP Nassoro Sisiwayah amesema uamuzi huo umefuatia malalamiko ya abiria waliokuwa wanasafiri na basi hilo kukwama tangu jana Disemba 29 majira ya saa kumi jioni katika eneo la njia Panda ya Himo Moshi mkoani Kilimanjaro baada ya gari hilo kuharibika.

Sisiwayah amebainisha kuwa basi hilo ni kati magari yaliyopewa vibali vya muda na mamlaka ya udhibiti usafiri ardhini LATRA kutoa huduma katika kipindi hiki cha cha sikukuu ya mwisho wa mwaka kuelekea Kilimanjaro kutokana na wingi wa abiria.

Awali wakizungumza kwa njia ya simu na kituo cha habari cha EATV, mmoja wa abiria hao, Ally Bilali amasema baada gari hilo kuharibikawalipiga simu kwa mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Kilimanjaro na kujibiwa kuwa kwa mujibu wa sheria wanapaswa kusubiri ndani ya masaa sita ndipo hatua nyingine zichukuliwe.

Ameongeza kuwa walisubiri masaa sita lakini hakuna hatu zilizochukuliwa ndipo yeye pamoja na baadhi ya abiria wakalazimika kwenda katika Kituo cha Polisi Himo ambapo waliambiwa kuwa angekuja mkaguzi wa polisi kukagua gari hilo lakini hakufika.

Bilali amesema kuwa leo Disemba 30 alipaswa kuwa mahakamani Dar es salaam lakini bado amekwama akidai kukwamishwa kwa makusudi tangu jana na kubainisha kuwa angalau wanerudishiwa nauli au kutafutiwa gari nyingine kama ilivyo sheria za usafirishaji.

"Leo asubuhi inspector Mayunga ametuambia mmiliki hapatikani tuandike taarifa zetu na majina yetu tutafute usafiri tuondoke, atakapopatikana watatuita turudishiwe gharama zetu, kuna wengine hamudu hizo gharama, sijui inakuwaje", ameongeza.

Afisa mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini, LATRA mkoa wa Kilimanjaro, Paul Nyello amesema taarifa hiyo ya malalamiko ya abiria wameipokea leo saa mbili asubuhi na kutafuta usafiri mbadala, baada ya dereva na kondokta kukimbia huku mmiliki akishindwa kutoa ushirikiano baada ya kutafutwa kwenye simu na kujulishwa tatizo la basi lake kabla ya simu yake kutopatikana tena ikidhaniwa kuwa aliizima kabisa.