Tuesday , 30th Dec , 2025

“Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe lilianza mara moja uchunguzi na ufuatiliaji wa kina kwa kutumia taarifa za kiintelijensia ili kuwabaini na kuwakamata wahusika wa tukio hilo".

Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe limethibitsha vifo vya watu wanne wanaodaiwa kuwa ni majambazi ambao wamehusika katika tukio la mauaji  Wiliam Mwampashi (45), mlinzi, ambaye alishambuliwa kwa kutumia kitu chenye ncha kali.

 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Augustino Senga amesema tukio hilo limetokea leo Disemba 30, 2025 ambapo majira ya saa 09:30 alfajiri, liliripotiwa tukio la mauaji ya Wiliam Mwampashi (45), mlinzi wa duka la simu na huduma za kifedha linalomilikiwa na Gabriel Nsemwa, lililopo katika eneo la Stand Kuu ya Vwawa, Kata ya Ichenjezya, Wilaya ya Mbozi, Mkoa wa Songwe.

“Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe lilianza mara moja uchunguzi na ufuatiliaji wa kina kwa kutumia taarifa za kiintelijensia ili kuwabaini na kuwakamata wahusika wa tukio hilo,“ amesema.

Ameongeza kuwa, katika hatua za ufuatiliaji, askari waliwafuatilia watuhumiwa hadi eneo la Ilembo, ambako waliwakuta wakiwa ndani ya nyumba, wakati wa utekelezaji wa majukumu yao, kulitokea majibizano ya mashambulizi ya risasi kati ya askari na majambazi.

Katika tukio hilo, askari walifanikiwa kuwajeruhi majambazi wanne (4) ambao walifariki wakati wanapatiwa matibabu katika Hospital ya Wilaya ya Mbozi ambao ni Eliuta @Mapunda, Abdul @Chiba, Justine na Bruce Mwasenga wote wanne wakiwa na historia ya kuwahi kufungwa miaka 30 jela kwa makosa ya mauaji na unyang’anyi kwa kutumia silaha na waliachiwa kwa rufaa.

“Watuhumiwa hao walikuwa wanafanya matukio hayo katika Mikoa wa Mbeya, Songwe, Rukwa na Katavi. Katika eneo la tukio askari walipata mali mbalimbali walizoiba katika duka hilo ambazo ni: Simu janja 30, Simu ndogo 172, Mashine ya POS 01 ya Benki ya CRDB, Bastola ya kutengenezwa kienyeji 01, Mtalimbo wa kuvunjia 01, Bisibisi 04 na risasi 04 na ganda 01 la risasi ikiwa ni pamoja na Nondo za kuvunjia milango na makufuli 02.“ Kamanda Senga amesema.

Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi, kuendelea kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za kihalifu au uhalifu wowote kwa Jeshi la Polisi lilisisitiza kuwa linaendelea na msako mkali wa kuwatafuta watuhumiwa wengine waliohusika na tukio hilo ili wachukuliwe hatua kali za kwa mujibu wa sheria.