Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Divisheni ya Ardhi, leo Disemba 31 itasikiliza maombi ya dharura katika shauri la maombi madogo ya Ardhi namba 32609 la mwaka 2025, linalomhusisha Miriam Solomon dhidi ya Azm Dewji na wadaiwa wengine wanne.
Katika shauri hilo, Miriam Solomon anafungua kesi akiwa kama msimamizi wa mirathi ya marehemu Solomon Sumai. Maombi hayo yamewasilishwa chini ya hati ya dharura, yakiiomba Mahakama itoe Amri ya Mareva, ambayo inalenga kudumisha hali ilivyo katika mali inayobishaniwa hadi shauri la msingi litakaposikilizwa na kutolewa uamuzi wa mwisho.
Chanzo cha mgogoro huo ni umiliki wa kiwanja namba 589, Kitalu kilichopo eneo la Kigamboni, ndani ya Manispaa ya Kigamboni, Jijini Dar es Salaam ambapo pande zote katika shauri hilo zinadai haki ya umiliki wa kiwanja hicho.
Mahakama inatarajiwa kusikiliza hoja za pande zote leo kabla ya kuamua iwapo itatoa amri ya muda ya kuzuia mabadiliko yoyote katika eneo hilo hadi kesi ya msingi itakapoamuliwa.

