Wednesday , 7th Jan , 2026

Wakristo wa Kanisa la Orthodox la Ethiopia hufuata kalenda ya Juliani (Julian Calendar), ambayo iko nyuma kwa siku 13 ikilinganishwa na kalenda ya Gregori inayotumiwa na Wakatoliki na Waprotestanti.

Leo Januari 7 raia wa Ethiopia wanasherehekea Krismasi baada ya Maelfu ya Wakristo wa Kanisa la Orthodox, wakiwa wamevalia mavazi meupe, kuadhimisha mkesha wa Krismasi katika Uwanja wa Meskel jijini Addis Ababa jana Jumanne Januari 6, 2026.

Sherehe hiyo ya kuwasha mishumaa katika mji mkuu wa Ethiopia ilifuatiwa na ibada ya kanisani iliyodumu usiku kucha, ikiashiria kumalizika kwa siku 43 za mfungo.

Wakristo wa Kanisa la Orthodox la Ethiopia hufuata kalenda ya Juliani (Julian Calendar), ambayo iko nyuma kwa siku 13 ikilinganishwa na kalenda ya Gregori inayotumiwa na Wakatoliki na Waprotestanti.

Ethiopia kwa ujumla imekumbwa na changamoto za amani mwaka uliopita wa 2025 ambapo licha ya vita katika eneo la Tigray kumalizika mwaka 2022, maeneo mawili makubwa zaidi ya nchi hiyo, Amhara na Oromia, yanakabiliwa na waasi wa misingi ya kikabila wanaotishia usalama wa ndani.

Licha ya changamoto hizo, Addis Ababa imeendelea kustawi baada ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed Ali kutumia mabilioni ya dola katika kuuboresha mji huo, ikiwemo ujenzi wa njia za baiskeli, kituo cha mikutano, bustani na makumbusho katika taifa ambalo linatarajia kufanya uchaguzi mkuu mwezi Juni mwaka huu wa 2026.