Wananchi wa Kijiji cha Msandamuungano, Kata ya Msandamuungano, Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa, wameiomba Serikali kuwapatia msaada wa haraka kufuatia dhoruba kali iliyosababisha uharibifu mkubwa wa makazi na kuwaacha baadhi ya wakazi bila hifadhi.
Wakizungumza na #EATV Baadhi ya wananchi akiwemo Neema Martin, wamesema kuwa dhoruba hiyo iliyotokea Januari 04, ikihusisha mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali, na kusababisha maafa yaliyoharibu nyumba na mali za wakazi wa kijiji hicho.
Mwenyekiti wa Kijiji, Sauli Nkolekwa, amethibitisha tukio hilo na kueleza kuwa jumla ya kaya 17 zimeathirika, huku watu wawili wakijeruhiwa na kukimbizwa hospitalini kwa matibabu.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Dr. Atman, Dkt. Magaka, amesema kuwa hospitali ilipokea majeruhi wawili baba na mtoto, ambao baada ya kupatiwa matibabu na hali zao kuimarika, waliruhusiwa kurejea nyumbani.
Diwani wa Kata ya Msandamuungano, Reus Kosam Mnyalika, amesema Serikali inaendelea na tathmini ya athari, sambamba na kutoa elimu kwa wananchi juu ya mbinu za kujikinga na majanga ya asili. Amebainisha kuwa, licha ya uharibifu huo, hakuna mtu aliyepoteza maisha.






