Thursday , 8th Jan , 2026

Mtuhumiwa huyo aliyeishi Tanzania tangu 2023, alitumia biashara ya kuuza chai ya maziwa kuficha biashara ya dawa za kulevya anayoifanya.

Jefferson Kilonzo Mwende (35), raia wa Kenya amekamatwa na Mamlaka ya kudhibiti na Kupambana na dawa za kulevya akiwa na gramu 131.88 za heroin katika operesheni iliyofanyika Sinza C mtaa wa Bustani nyumba namba 16.

Mtuhumiwa huyo aliyeishi Tanzania tangu 2023, alitumia biashara ya kuuza chai ya maziwa kuficha biashara ya dawa za kulevya anayoifanya.

Aidha, Mamlaka hiyo katika oparesheni zake katika mtaa wa Wailes, Temeke, Dar es Salaam, imefanikisha kukamatwa kwa pakiti 20 za skanka zenye uzito wa kilogramu 20.03 zikiwa zimefichwa ndani ya balo la mitumba na kufichwa kwenye bus aina ya Scania la kampuni ya King Masai Tours, lenye namba za usajili wa nchi ya Msumbiji namba AAM 297 CA.

Bus hilo hufanya safari zake kati ya Nampula nchini Msumbiji na Tanzania na Watuhumiwa waliokamatwa kuhusiana na tukio hilo ni Amasha Iddi Mrisho (40), mkazi wa Buza, Dar es Salaam na Seleman Juma Ally (32), raia wa Msumbiji.