Jeshi la Polisi mkoa wa Pwani, linamshikilia Agnes Liku (35), mkazi wa Kijiji cha Mwanzomgumu, Kata ya Msimbu Wilaya ya Kisarawe, kwa kutoa taarifa za uongo, kuwa amejifungua mtoto katika zahanati ya kijiji hicho na mtoto kuchukuliwa na ofisa tabibu asiyefahamika.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Salim Morcase, amesema mnamo Januari 6, 2026 saa 12 jioni, Agnes alisema alienda katika zahanati hiyo ya kijiji akiwa na rafiki yake Eveline Mazigo na alipofika katika zahanati hiyo alieleza kuwa ana uchungu wa kujifungua hivyo ofisa tabibu, Tatu Nyahoza alimpokea na kumpima.
Baada ya vipimo, Agnes alibainika kuwa njia ya uzazi haijafunguka kuruhusu mama huyo kujifungua.
Kwa mujibu wa Kamanda Morcase, mnamo majira ya saa tatu usiku walifika ndugu Maduki Shabani na Catherine Raphael katika zahanati hiyo kumsaidia Agnes ambaye alijieleza kwamba anasubiri kujifungua.
Hata hivyo, inadaiwa kuwa majira ya saa saba usiku, Agnes aliwaita ndugu akiwa chumba cha kujifungulia na kuwaeleza kwamba amejifungua na tabibu aliyemhudumia ameondoka na mtoto.
Ndugu walimuita tabibu Tatu Nyahoza aliyekuwa chumba cha jirani ambaye alimpima tena Agnes na kubaini njia bado haijafunguka kuruhusu kujifungua isipokuwa aliona damu.
Tatu alivyoona sintofahamu hiyo aliamua kutoa taarifa kwa uongozi wa Kitongoji na kuripoti kwa Jeshi la Polisi kupitia Polisi Kata ya Msimbu. Upelelezi wa jalada hilo tayari umekamilika na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.



