Wednesday , 14th Jan , 2026

Mkuu wa Tume ya Uchaguzi nchini Uganda amesema ametishiwa maisha juu ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi.

Bw Simon Byabakama alikuwa akijibu swali la wanahabari kuhusu klipu ya video mtandaoni ambapo msaidizi mkuu wa rais amenukuliwa akidai kuwa Tume ya Uchaguzi haitawahi kumtangaza mgombea wa upinzani Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine, kuwa rais.

Katika video hiyo, Msaidizi Maalum wa Rais wa Utoaji Huduma na Ufuatiliaji, Bw Yiga Kisakyamukama, anasikika akisema, "Usitarajie, hata usifikirie, kwamba Simon Byabakama anaweza kumtangaza Bobi Wine. 

Msaidizi huyo aliongeza kuwa Rais Museveni, ambaye yuko madarakani, atasalia uongozini

Bw. Byabakama alisisitiza kuwa Tume hiyo iko huru kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na kusisitiza kuwa itamtangaza mshindi kwa misingi ya hesabu ya kura.

Aliendelea kufichua kuwa watu fulani walikuwa wamemwonya kwamba ikiwa atashindwa kutangaza wagombeaji mahususi kama washindi, kuna athari fulani zitakazomkabili.

Amesisitiza kuwa hana wasiwasi na kusema anaendelea kuzingatia kutekeleza majukumu yake kwa watu wa Uganda.

Bw Byabakama alisisitiza kuwa Uganda itasalia kuwa nchi salama hata baada ya uchaguzi.

Raia wa Uganda wanatarajiwa kupiga kura tarehe 15 Januari kumchagua rais na wabunge.