Monday , 26th Jan , 2026

Rapper maarufu kutoka Canada, Drake, ameendelea kuandika historia katika muziki wa HipHop baada ya kufanikisha rekodi kubwa ya kuwa msanii wa kwanza wa HipHop duniani kufikisha wasikilizaji bilioni 4 kwenye mtandao wa kusikilizia muziki Spotify.

Pichani ni Drake na WizKid

Rekodi hii inaonesha ukubwa wa ushawishi wa Drake katika muziki wa kimataifa, pamoja na nguvu ya mashabiki wake waliopo kila kona ya dunia. Kwa zaidi ya muongo mmoja, Drake ameendelea kutawala chati, kuvunja rekodi za streaming na kuachia nyimbo zinazodumu muda mrefu sokoni.

 

Moja ya ngoma zilizochangia kwa kiasi kikubwa mafanikio haya ni “One Dance”, wimbo uliotoka mwaka 2016 kupitia album ya Views. Licha ya kuwa na zaidi ya miaka tisa (9) tangu ulipotoka, One Dance bado unaendelea kusikilizwa kwa wingi hadi leo.

Ngoma hii pia inabeba sauti ya msanii kutoka Nigeria, Wizkid, ambaye anatajwa kuwa miongoni mwa waandishi wa wimbo huo. Ushirikiano huu uliifanya One Dance kuwa daraja muhimu kati ya HipHop, Dancehall na Afrobeats, na kuipa Afrobeats nafasi kubwa katika soko la kimataifa.

 

Kupitia One Dance, Drake na Wizkid waliweka alama isiyofutika katika historia ya muziki wa dunia. Wimbo huo uliwahi kushika nafasi ya kwanza kwenye chati mbalimbali, ukiwemo Billboard Hot 100, na kuwa miongoni mwa nyimbo zinazostreamiwa zaidi muda wote.

Rekodi ya Drake kufikisha wasikilizaji bilioni 4 Spotify si tu ushindi wake binafsi, bali ni ushahidi wa namna muziki wa HipHop na Afrobeats ulivyokua na kuvuka mipaka ya kijiografia.