Jumatatu , 17th Apr , 2023

Zaidi ya wafanyabiashara 62 waliokuwa wakifanya biashara zao katika soko la Kigogo Luhanga jijini Dar es Salaam, wamevunjiwa vibanda vyao kwa kile kilichodaiwa kwamba wamekuwa wakifanya biashara kwenye eneo hilo kinyume na sheria ambalo wamelivamia na ni mali ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Mabaki ya vibanda vilivyobomolewa

Vibanda hivyo vimevunjwa alfajiri ya leo Aprili 17, 2023, na serikali, ambapo wafanyabiashara hao wamesema wamevunjiwa bila kupewa taarifa hali iliyopelekea kupata hasara kwani wengi wao walikuwa wakilaza bidhaa zao sokoni hapo.

Wakizungumza na EATV katika eneo hilo wafanyabiashara hao wamesema kuvunjiwa kwa  mabanda yao bila kupewa taarifa Ili wajiandae kwa kuondoa mali zao kumesababisha wapate hasara kwa kupoteza mali zao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa soko hilo akizungumza amesema hali za wafanyabiashara hao kwa sasa kiuchumi zimekuwa mbaya kwani mitaji ya biashara zao imepotea kwa kuwa bomoa bomoa hiyo haikuzingatia wala kujali mali zilizokuwepo ndani ya soko na hivyo kuamua kubomoa na kuharibu mali hizo

Naye Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Matokeo, Kata ya Mabibo ambako ndiko soko hilo lipo Mfaume Mohamedi amesema kuvunjwa kwa soko hilo ni matokeo ya ushindi walioupata mahakamani  CCM ambao walifungua kesi ya kudai eneo lao na kushinda kesi hiyo.