
Aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad.
Taarifa ya kifo cha Maalim Seif, ilitolewa na Rais wa Zanzibar Dkt Hussein Mwinyi, mnano Februari 17, 2021, na kueleza kwamba mauti yamemfika wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, jijini Dar es Salaam.
Maalim Seif alifariki dunia akiwa ametumikia nafasi hiyo ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa chini ya siku 100, akiwa sehemu ya serikali ya umoja wa kitaifa iliyoundwa baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Kufuatia taarifa za kifo chake, viongozi mbalimbali wa serikali, vyama vya siasa na mataifa mengine mbalimbali walitoa pole kwa familia na taifa kwa ujumla kwani Maalim Seif, alikuwa kiongozi kiunganishi mkubwa, mwenye upendo, hekima na aliye mwalimu mzuri kwa waliokuwa karibu naye.
Maalim Seif alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 77, na alikuwepo kwenye siasa za Zanzibar tangu miaka ya 1970, akiwa Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi na Waziri wa Elimu kati ya 1977 – 1980, na mjumbe mwazilishi wa baraza la wawakilishi visiwani humo.