Alhamisi , 22nd Nov , 2018

Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Mayunga Samwel mkazi wa Mtaa wa Mkudi Wilayani Ilemela Mkoani Mwanza  amekutwa akiwa amejinyonga chumbani kwake kwa kutumia shuka.

Picha haihusiani na tukio.

Marehemu huyo amejinyonga kwa kile kilichosadikika kuwa alikua akimtaka mwanae mwenye umri wa miaka 2 ambaye alikua ameondoka na mke wake baada ya wanandoa hao kutengana ila yeye alikua akimtaka mtoto huyo kwa miezi 11 ili aendelee kuishi naye.

Mwenyekiti wa mtaa wa Mkudi Sebastian Mkunda amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kudai kuwa kabla ya kifo cha marehemu alikuwa na malalamiko ya kudai mwanae kutoka kwa mke wake waliokuwa wameachana kwa muda mrefu.

Siku moja kabla ya mauti kumkuta kijana huyo inadaiwa alikua akilalamika kwa majirani zake kuhusu kuwa mbali na mwanae baada yeye na mkewe  kutengana.

Mwili wa marehemu Mayunga umechukuliwa na jeshi la Polisi kwaajili ya Uchunguzi zaidi.