
Akizungumza na waandishi wa habari majeruhi wa tukio hilo ambaye amelazwa hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga amesema alikuwa anatembea njiani akielekea nyumbani ghafula alivamiwa na kundi la watu wakiwa na visu na mapanga na kuanza kumshambulia wakimtaka awape hela ndipo walichukuwa simu na fedha alizokuwa nazo.
Amesema alijaribu kupambana na watu hao ambao asilimia kubwa walikuwa ni vijana lakini alizidiwa nguvu,baada ya kumkata panga kichwani na miguuni na kuanguka chini huku akipiga kelele za kuomba msaada ndipo walijitokeza baadhi ya wananchi kumsaidia huku waliofanya tukio hilo walikimbia na kutokomea kusikojulikana.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Burugalila amesema amepata taarifa ya tukio hilo na kutoa taarifa mamlaka husika kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria huku akiwataka wananchi kuacha kutembea nyakati za usiku kwa ajili ya usalama wao.
Kwa upande wake Kaimu Mganga mfawidhi hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga Dkt.Kambi Buteta,amethibitisha kumpokea majeruhi huyo akiwa na majeraha kichwani,mikononi na kwenye miguu yakionyesha amejeruhiwa na kitu chenye incha kali huku damu zilikuwa zikimwagika nyingi na kuanza kupatiwa huduma haraka.
Jeshi la polisi Mkoani Shinyanga bado linaendelea na uchunguzi zaidi wa tukio hilo.