
Kamanda Mambosasa.
Kamanda wa polisi kanda maalum ya Dar es salaam, Lazaro Mambosasa amesema tukio hilo lilitokea Machi 3 mwaka huu na kwamba askari huyo wa JWTZ alikiri kumiliki silaha mbili na kuzitumia kwenye matukio ya uhalifu katika maeneo mbalimbali ya mikoa ya Dar es salaam na Pwani.
Amesema wakati akihojiwa, askari huyo aliwaambia polisi kuwa alikuwa akizihifadhi silaha nyumbani kwa mke wake mdogo mkoani Pwani. Mambosasa amesema polisi walifika kwenye nyumba hiyo na kukamata silaha aina ya AK 47 yenye namba NM 174844 ikiwa na risasi 20, boksi lenye risasi 27 na bastola yenye namba 3249 ikiwa na risasi saba na risasi nyingine tatu za silaha ya G3.
“Mtuhumiwa alikubali kuwaonyesha wenzake watatu anaoshirikiana nao, askari walipofika kwenye nyumba wanayoishi watuhumiwa hao walianza kukimbia kupitia mlango wa nyuma, ambapo tukio hilo liliwafanya askari warushe risasi hewani kuwaamuru wasimame lakini wakakaidi ndipo walipowafyatulia risasi ambazo ziliwajeruhi na walifariki dunia njiani wakipelekwa hospitali,”, amesema Kamanda Mambosasa.