Jumatatu , 6th Apr , 2015

UFINYU wa bajeti na upungufu wa wataalam wa misitu, umesababisha Mkoa wa Arusha kushindwa kufikia malengo ya kupanda miti milioni kumi kila mwaka, kwa miaka mitatu mfululizo ili kukabiliana na uharibifu wa mazingira, unaochangia kuwepo na mabadiliko

Hayo yamesemwa siku ya maadhimisho ya siku ya upandaji miti mkoa wa Arusha ,Julius Achiula, wakati alipokuwa Wilayani Longido

Achiula, amesema mkoa umejipangia kupanda miti milioni 10 kila mwaka, lakini kutokana na changamoto mbalimbali zikiwemo ufinyu wa bajeti, upungufu wa wataalam katika mamlaka ya serikali za mitaa, mwamko mdogo wa wananchi upandaji miti umeshindwa kufikia lengo.

Achiula, amesema mwaka 2013/14 mkoa ulipanda miti milioni 5.4 tu sawa na asilimia 52% ya lengo la kupanda miti milioni kumi, na mwaka 2014/15 mkoa ulipanda miti milioni 7.4 sawa na asilimia 70% ya lengo la kupanda miti milioni 10.5 kwa mwaka.

Amesema ni halmashauri ya Arusha, pekee ndio imefanikiwa kupanda miti mingi katika mkoa kwa kupanda miti milioni 1.4 kati ya lengo la kupanda miti milioni 1.5.

Ametaja changamoto zinazokwamisha kutekelezwa kwa lengo hilo, ni mwamko mdogo wa jamii, uvamizi wa misitu na uharibifu wa maeneo ya misitu kutokana na ongezeko la shughuli za kibinadamu, uvunaji haramu wa misitu, upungufu wa vitendea kazi na wataalam, mabadiliko ya tabia nchi.

Changamoto nyingine ni uchimbaji haramu wa madini kwenye maeneo ya misitu, makundi makubwa ya ng’ombe yanayoharibu misitu, uchomaji moto unaosababishwa na wawindaji na walina asali kwenye misitu.

Achiula, amesema katika kukabiliana na changamoto hizo,mkoa unashirikiana na mamlaka ya serikali za mitaa wizara ya maliasili na utalii na sekta binafsi, kushirikiha jamii katika kuhifadhi misitu.

Naye Mkuu wa mkoa wa Arusha, Daudi Ntibenda, ameagiza viongozi wa Wilaya ya longido kuiga mfano wa shule ya Sekondari Longido kwa kutunza mazingira licha ya ukame walionao, ili kunusuru uharibifu wa mazingira wilayani humo.

Ntibenda amesema kutokana na tathmni ya raslimali ya misitu nchini, iliyofanywa na wizara ya maliasili na utalii, kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2009 hadi 2014 nchi imepoteza hekta 372,000 za misitu na kusababisha kuwepo asilimia 70 % kiasi kikubwa cha hewa ya ukaa angani.