Ijumaa , 16th Dec , 2022

Balozi wa Tanzania nchini China Mbelwa Kairuki amesema moja ya watu waliomfundisha masuala ya diplomasia ni aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Austria, Celestine Mushy ambaye amefariki mwanzoni mwa wiki hii

Balozi Kairuki ameyasema hayo wakati akizungumza na EATV kuhusu jinsi alivyomfahamu balozi huyo na jinsi walivyoshirikiana katika kuipigania Tanzania kimataifa

"Tulikuwa pamoja pale wizara ya mambo ya nje kama maafisa na mimi nilimkuta, wakati mimi nilipojiunga na wizara yeye alikuwa ubalozi wa umoja wa mataifa, kwa mara ya kwanza tulikutana Marekani na alinipokea vizuri na kunifundisha masuala ya umoja wa mataifa" amesema Balozi Kairuki ambaye ni balozi wa Tanzania nchini China
Balozi huyo wa Tanzania nchini China amesema watanzania na dunia itamkumbuka balozi Mushy kwa uzalendo wake na uchapakazi wake mkubwa 

"Alikuwa anapenda kumuelewesha kila mtu aelewe, alikuwa mwalimu mzuri sana na mzalendo, watu ambao wamefanyanaye kazi watamkumbuka jinsi ambavyo alikuwa akitaka kila mtu aelewe na kuwapa changamoto" ameeleza balozi Kairuki

Aidha Balozi Kairuki amesema kwa mara ya mwisho walikutana Zanzibar katika mkutano wa mabalozi na alikuwa na michango mizuri sana ya kulenga kuboresha zaidi diplomasia ya nchi na utendaji ndani ya wizara ya mambo ya nje
Balozi Celestine Mushy alifariki katika ajali mkoani Tanga wilayani Handeni wakati akiwa safarini akiendesha gari mwenyewe

Mwili wa Balozi Mushy unatarajiwa kuzikwa Jumanne Desemba 20, 2022 nyumbani kwake Moshi mkoani Kilimanjaro