Jumapili , 9th Oct , 2016

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amepatiwa tuzo za uendelevu wa tabianchi kutokana na harakati zake za kuchagiza mikakati ya kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon

Amekabidhiwa tuzo hiyo huko Reykjavic, Iceland wakati wa mkutano wa kila mwaka wa jumuiko la Arctic, ncha ya kaskazini mwa dunia ambapo katika hotuba yake amesema tuzo hiyo kwa niaba ya Umoja wa Mataifa, mashirika ya kiraia na wadau wote waliosimama kidete kutetea tabianchi.

Ban ametumia hotuba hiyo kuzungumzia mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi akisema hadi leo nchi 191 zimesharidhia na vigezo vyote viwili vimevukwa na mkataba utaanza rasmi mwezi ujao kama ilivyokwishatangazwa.

Katibu Mkuu akasema ni vema kutekeleza ahadi kwani mabadiliko ni dhahiri akitolea mfano eneo la ncha ya kaskazini akisema kiwango cha ongezeko la joto ni kikubwa kuliko kwingineko duniani hivyo maneno sasa yawe matendo.