Jumanne , 2nd Mei , 2023

Bibi wa miaka 63 pamoja na wajukuu zake wawili wamefariki dunia kwa kusombwa na maji ya mvua yaliyobomoa nyumba yao katika mtaa wa Bomani wilayani Tarime mkoani Mara, baada ya mto kufurika kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha mkoani humo.

Nyumba iliyosombwa na maji

Baadhi ya wakazi wa mtaa huo wamesema vifo hivyo vimetokea kwa kuwa bibi na wajukuu zake walikuwa wakiishi pembezoni mwa mto na kuiomba serikali kuwaondoa baadhi ya wanachi ambao nao wamejenga ndani ya eneo hilo la mto ili kuepusha vifo vingine kutokea.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto mkoa wa Mara Agustino Magere, amewataja waliofikwa na umauti huo kuwa ni Ghati Mwita 63 pamoja na wajukuu zake wawili ambao ni Jonson Denis miaka 10 na  Violet Denis miaka 3 

Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mzee, amefika katika eneo la tukio na kujionea hali halisi kisha akatoa maagizo kwa mkuu wa wilaya kufanya uchunguzi kama kuna watu wanaoishi kando ya mto huo waondolewe na kufutiwa hati zao.