Ijumaa , 6th Feb , 2015

Bunge limetakiwa kutoa azimio la kusitisha zoezi la utoaji wa vibali kwa raia wa kigeni kuishi, kufuga na kumiliki ardhi pamoja na kufuta vibali vyote vilivyopo na kuwataka raia wa kigeni wenye vibali hivyo kuondoka nchini mara moja.

Christopher Ole Sendeka

Akiwasilisha Bungeni taarifa ya kamati teule iliyoundwa kuchunguza na kuchambua sera mbalimbali zinazohusu masuala ya ardhi, kilimo, mifugo, maji na uwekezaji ili kubaini kasoro zilizomo katika matumizi ya ardhi, Christopher Ole Sendeka amesema idara ya uhamiaji inahusika kwa kiasi kikubwa kutoa vibali kwa wageni bila ya kufuata utaratibu na kutaka vibali vyote vilivyopo vifutwe na wageni hao kuamriwa kuondoka nchini.

Aidha kamati hiyo teule imeirushia lawama serikali kwa kutokuwa na nia ya dhati ya kumaliza migogoro ya ardhi nchini licha ya watendaji wake kuwa na taarifa zote zinazohusu migogoro ya ardhi nchini.

Wakichangia mara baada ya kamati hiyo teule kuwasilisha taarifa yake bungeni baadhi ya wabunge wamehoji sababu ya serikali kutochukua hatua kwa baadhi ya viongozi wa serikali na wawekezaji wa kigeni wanaotwaa maeneo makubwa ya ardhi na kisha kuwakodishia wananchi kwa bei kubwa.

Akizungumza mara baada ya kuwasilishwa kwa kamati hiyo spika wa bunge hilo amewataka wabunge kuachana na itikadi za kisiasa wakati wa kujadili masuala ya kitaifa na kuwataka wabunge kuacha kulalamika na kufanya kazi yao ya kuisimamia serikali kwa manufaa ya wananchi.