
Profesa Assad ametoa kauli hiyo kwenye mkutano wake na waandishi wa habari ikiwa ni saa chache baada ya Spika Ndugai kusema ni lazima kiongozi huyo afike kwenye kikao cha kamati ya maadili ili kujibu madai ya kauli yake.
Assad amesema, " mpaka hivi sasa ninaamini nina mahusiano yenye tija kati yangu na Bunge zima na lazima uhusiano huu tuuenzi, na majibu yangu ya kuwa dhaifu ni ya kawaida na hayakuwa na nia ya kudhalilisha Bunge."
"Maneno kama udhaifu, au mapungufu ni lugha za kawaida sana kwa wakaguzi katika maoni ya utendaji na mifumo kwenye taasisi mbalimbali ndiyo maana kwenye ripoti zangu nimelitumia mara kwa mara", ameongeza CAG.
Aidha Kiongozi huyo ameeleza kuwa Januari 21 atafika mbele ya kamati ya maadili ya Bunge ili kueleza madai yanayomkabili kama barua alivyoipokea januari 15 mwaka huu.