
Kwenye ukurasa wake wa facebook CHADEMA imeandika ikisema kwamba ni wakati muafaka kwa serikali ya Tanzania kurudisha mchakato wa Katiba mpya, ili kuweza kupata Katiba itakayo tenganisha mamlaka, na kulinda sheria za uchaguzi.
"Kutokana na historia hiyo ya kipekee iliyoandikwa na majirani zetu wa Kenya kupitia Mahakama ya Juu, CHADEMA tunashauri kwamba ni wakati mwafaka sasa Tanzania tukarejea katika mchakato wa kupata Katiba Mpya na yenye kuweka taasisi imara, Katiba ambayo Watanzania wanaitaka, na iweke kipengele cha matokeo ya urais baada ya uchaguzi mkuu kuhojiwa mahakamani", iliandika CHADEMA.
CHADEMA iliendelea kuandika kwa kutaka Katiba Mpya itakayopatikana iunde Tume Huru ya Uchaguzi na ambayo pia itaweza kushtakiwa mahakamani, pale ambapo itakiuka sheria za uchaguzi ili kuweza kuwa na uchaguzi huru na haki.
Kwenye ujumbe huo CHADEMA ilihitimisha kwa kuwataka Watanzania waamshwe na kitendo cha Mahakama ya Juu ya nchini Kenya, ili waweze kudai Katiba mpya na ambayo itaweka misingi imara ya taasisi nchini.
