Jumatatu , 3rd Apr , 2023

Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia  Idara ya Mambo ya Kale imeanza mkakati maalum wa  kuainisha, kuhifadhi na kuyatangaza maeneo ya kihistoria yanayopatikana katika Jiji la  Dodoma kwa lengo la kulifanya Jiji hilo kuwa na vivutio vya kila aina kama ilivyo katika Majiji mengine duniani

Hatua hiyo inakuja kufuatia kauli aliyoitoa siku chache zilizopita,  Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohammed Mchengerwa kuwa Tanzania imebariki kuwa na  vivutio vya utalii vya kila aina mbali na wanyamapori na kama kila Mtumishi atawajibika ipasavyo idadi ya watalii ifikapo mwaka 2025 itaongezeka maradufu.

Mkurugenzi wa Idara ya Mambo Kale, Dkt.Christowaja Ntandu  ametembelea maeneo ya Kihistoria yaliyopo Jijini  Dodoma  kama sehemu ya kufanikisha azma hiyo 

Akizungumza mara baada ya kutembelea Makaburi ya Wahanga wa Vita vya Kwanza na vya Pili vya Dunia,  Eneo la mnara wa Uhuru,  Mnara wa Mashujaa wa Tanzania, Nyerere square na Hoteli ya Dodoma, Dkt.Ntandu amesema ziara hiyo ni mkakati maalum wa kushirikiana Wadau wa Utalii katika Jiji hilo kwa lengo la  kuongeza mazao mapya  ya Utalii hususan utalii wa Malikake kwenye maeneo mbalimbali nchini  kuanzia ngazi ya kata mpaka Mkoa
Maeneo mengine aliyotembelea   ni pamoja na  eneo Kikuyu ambalo lina   asili ya jina la Dodoma, Mti aina ya Mkuyu  uliopo katika eneo la  Chuo Kikuu cha St. John ambao  ulitumika  kunyongea  wahalifu wakati wa Utawala wa Wajerumani

Akizungumzia Hoteli ya Dodoma ambayo licha ya kujengwa  mwaka 1901 lakini bado ipo kwenye hali nzuri, Dkt.Ntandu amesema  sehemu ya jengo hilo ikiwemo vyumba vya kulala wageni na baadhi ya vifaa vikiwemo meza na viti bado vinaendelea kutumika kutokana na  uimara wake.

Kwa upande wake,  Meneja wa Hoteli hiyo, Wellington Malea amesema  kuwa wataendelea kuhifadhi hoteli hiyo ili iendelee kuwa  kivutio kwa wageni kutoka ndani na nje ya nchi hususani Watalii  kutoka Nchi ya Ujerumani kwa kuwa  hoteli hiyo ilijengwa kipindi cha utawala  wa Wajerumani wakati wakijenga Reli ya kati.

Katika ziara hiyo Mkurugenzi Christowaja Ntandu aliongozana na timu ya watalaamu wake wa Malikale, Afisa Utamaduni na Afisa Utalii  wa Jiji la Dodoma.